 |
Aliyekua katibu wa Chadema Mbeya, Edo Makata
|
Ndugu waandishi,
Niruhusu niorodhesha sababu zinazoniondoa CHADEMA kuamua kuwa huru hadi hapo nitakapotangaza ama kuendelea na siasa au nabaki kuwa mtumishi wa taasisi ninakofanyia kazi na ujasiliamali wangu.
1. Bado sikubaliani na Ndugu Slaa kuwa na kadi ya CCM. Nataka airudishe ama awajibike kisiasa.
2. matumizi ya Ruzuku si sahihi. Mikoa, Wilaya, kata hawapewi pesa zaidi ya wao kujichangisha. Huku Maafisa wa makao Makuu wakiishi kama wafalme na Malkia.
3. Mgawanyo wa rasilimali za chama ni utata mtupu, Mkoa kama Mbeya, wenye CHADEMA ya kweli kwa sasa haujapewa hata kipaza sauti wakati magari yote na vifaa vyote vimehodhiwa na Makao Mkuu, hii ni zaidi ya ufisadi tunaopiga kelele. Kuwafanya wanachama wa Mikoani ni kuku wa kienyeji kwa kuwarushia punje za mchele unapotaka kuwachinja. Mikoani viongozi na wanachama wanatoa pesa zao kwa kujichangisha kwa imani kuwa siku moja watakula keki ya Ruzuku na ufadhili. Mimi nawahakikishia , kwa unyenyekevu nilioufanya hawatopata hadi Mbowe na Slaa watoke kwenye nafasi walizo nazo kwa sasa. Wasidanganywe na siasa za mikutano ya matumaini ya kitaifa yenye posho.
3. Mfumo wa Demokrasia ndani ya chama haufanani na kelele tunazozipiga kwa wananchi wengi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu (3K), Kimsingi CHADEMA tunauhaba wa Demokrasia. Mfano:
(i) Mchakato wa mgombea uraisi (2010) ndugu Slaa kamati kuu ilipendekeza jina lake na kuitisha Baraza kuu na mkutano mkuu Tukavumilia.
(ii) Wagombea ubunge nikiwemo mimi tulitumana tu kwenye majimbo kwa lengo la kuibana CCM- tumevumilia. Viti maalum, tumevumilia. Sasa hivi ukitaka kugombea jimbo unatakiwa kuandika barua makao Makuu;, huu ni utawala wa ki-ubwenyenye ndani ya chama kuwafanya wapinzani wako wakudhuru au wakuzidi kete kwa mbinu za kujuana makao Makuu.
(iii) Kitendo cha mwenyekiti wa chama Mhe,Freeman Aikael Mbowe (Mb) kiongozi wa kambi Rasmi ya upinzani kuropoka, eti Ndugu Slaa atakuwa ndiye ngombea uraisi mwaka 2015 ni cha kuua kabisa Demokrasia ndani ya CHADEMA. Tena ninamshauri bure kakangu ninayemheshimu kwa siasa zake; atubu kama aliwahi kumshambulia Yusuf Makamba alipokuwa katibu mkuu – CCM aliposhikilia bango, kuwa mgombea mwenye mtaji ni Jakaya Kikwete. Mbowe awaombe radhi wanachama na wananchi wapenda mabadiliko. Hawezi kuwaburuza wasomi kama prof. Baregu, Prof. Safari, Dk. Kitila Mkumbo na wengine wengi. Leo hii mimi ungeniuliza nani anafaa kuiendesha CHADEMA ngazi ya Taifa ningesema Dk. Kitila ni wakati wake wa kuacha kazi Serikalini na kuwa katiba mkuu wa CHADEMA. Hata kuingizwa kwenye mchakato wa ugombea nafasi za juu za nchi.
4. Migogoro isiyo na suluhu wa mlingano katika kuitatua. Mfano ni Mwanza na Arusha. CHADEMA imefukuza Madiwani, lakini Karatu nyumbani kwa Slaa wanabembelezwa, hapa pana ajenda ya kuifanya CHADEMA iwe ni SACCOS tu ya wajanja wachache. Kuna kundi linatafuna fedha za chama.
5. Maandamano ya kudai haki: Hata siku moja hayajaitishwa Moshi, Karatu ili nako wananchi wa kule waonje joto ya jiwe kupambana na polisi, Maandamano ni Mbeya, Mwanza, Arusha ambako viongozi wao wanafukuzwa wakiongea ukweli au kutoa hoja zenye mantiki.
6. Matumizi yasiyo sahihi ambapo Viongozi huomba mchango kwa wanachama halafu hutumia kadri wanavyoona inafaa jambo ambalo ni fedheha kubwa na wananchi ni lazima watambue haya.
Pia upandikizaji wa siasa za uchochezi katika Vyuo Vikuu ni hali iliyosababisha baadhi ya wanafunzi kufukuzwa na chama kutowasaidia kutatua migogoro yao na serikali, Uongozi wa Vyuo.
Ndugu waandishi,
Kuna hoja tunaendelea kuzilea ndani ya CHADEMA na hatimaye zimezaa ulemavu wa Demokrasia ya kibabe Mfano: Suala la Ukanda kuwa na nguvu Kaskazini lina nafasi yake. Hoja inafuatia manyanyaso ayapatayo Zitto Kabwe (Kigoma), Arfi Said (Rukwa), Shibuda (Maswa) Juliana Shonza (Mbeya), Naombi Kaihula (Mbeya), Nyimbo (Iringa).
Ndugu waandishi,
Dhambi hii ya dhana ya ubaguzi inajikita kwenye ubaguzi wa dini na ukabila. Leo hii Zitto na Arfi ni waislamu, CHADEMA haiwataki, na hao ndiyo nguzo ya Waislamu ndani ya CHADEMA haiwataki, na hao ndiyo nguzo ya Waislam ndani ya CHADEMA, ukiwaondoa tunabaki Wakristo tupu. Halafu unasema chama kiongoze ‘DOLA’ huu ni utani wa utawala kwa Taifa kama Tanzania.
Ndugu waandishi,
Kurugenzi zote nyeti Makao Makuu yaani za fedha, utawala, habari zimekamatwa na watu wa Kaskazini. Bado kelele za marehemu chacha waugue hazirekebishi pia kitabu alichoandika ndugu Deo hakiwafundishi lolote. Chama kimeendelea kuwa NGO.
Uwezo wa Slaa kuwa Mtawala ni mdogo, hupendelea kusikiliza majungu na huvutiwa na wanaomsifia tu. Watu kama mimi tunaojenga hoja hatupandwi na tunageuka maadui kwake na wapambe wao nawasihi waache ubabe, chama ni mali ya watanzania si chao pekee.
Hapa pana mchezo wa Pwagu na Pwaguzi mmoja kusema nina kadi ya CCM na mwingine kutangaza mgombea uraisi. Hawa viongozi wanaelewa wanachokisema, hawakosei. Chukulia usemi huo wa kukiri kuwa na kadi ya CCM ungewtamkwa labda na Zitto Kabwe au Shibuda. Kamati kuu ingetishwa na haraka wangefukuzwa dalili za kauli hizi ni ishara kwa Zitto Kabwe kuwa mawazo yake ya kulitumikia Taifa ndani ya CHADEMA yanasafari ndefu. Hatokaa salama kisiasa. Hao wakubwa wameamua kuua chama ama kujibinafsisha, maamuzi magumu ni kuwatoa wao, CHADEMA itayumba baadaye itasimama.
Ieleweke kuwa kupendwa kwa CHADEMA ni kwa sababu ya Watanzania wana haja ya kuona chama kingine kinatawala. Nani alimjua Slaa ndani ya CHADEMA tangu 1995 hadi 2007 kabla ya Zitto kutolewa nje ya vikao vya Bunge? Hoja ya Mafisadi aliyopewa – Mwembe Yanga ndiyo aliyomnyanyua hadi leo. Lakini je, yeye anamiliki mali zinazofanana na Utumishi wake kama Padri na baadaye Mbunge? Ajibu! Kwa nini hoja ya Ufisadi kaizima? Muulizeni mali zake ndani ya nchi na nje wanakoishi watoto wake (Uingereza).
Leo watu wa Mbeya tunaambiwa tumzomee Rais Kikwete tuchome barabara na kuharibu uchumi. Raisi wa nchi anaona Mbeya kama kisiwa, lakini Slaa anamwita Kikwetge CCBRT anamsifia sana, Mbowe anafanya kazi na Raisi kule Hai – Kilimanjaro anamsifia sana. Mbunge wa Mbeya Mjini anapayuka Bungeni Mbeya wanamkataa Raisi. Lazima watu wa Mbeya tushituke, tumwache Raisi afanye kazi ya kuleta Maendeleo maana ndiye aliyeapishwa ndiye aliyeshinda uchaguzi – akatangazwa.
Wote waliomkataa ndani ya Bunge wanashinda na safari za Ikulu kunywa naye chai huku Mbeya tunaambiwa mkataeni. Hapana. Hii michezo ya siasa za kidhalimu tuishitukie. Mbeya tunapuuzwa na Jiji letu litachelewa kupata Maendeleo yanayolengwa na Miji ya Arusha na Mwanza. Tuseme Slaa na Mbowe yatosha kuwatumia watu wa Mbeya kama mtaji wa maandamano.
Ndugu waandishi,
Mimi naifahamu vizuri CHADEMA, nimekuwa mgombea Udiwani 2005 (Kata ya Mabibo –
DSM) na mgombea ubunge Jimbo la Kyela – 2010. Nimekuwa kiongozi ngazi ya Mkoa
Mbeya – Katibu wa Mkoa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa. Pia nimeshika nafasi
kadhaa Mkoa wa Dar es salaam kabla ya kuja Mbeya. Hawa wana siasa wengi walio
ndani ya CHADEMA ni waganga njaa tu mle ndani ni wachache sana wanafikiri mageuzi
ya kiuchumi na utawala kwa taifa letu.
Hivyo nathibitisha mbele yenu kuwa hakuna mtu ndani ya upinzani na hasa CHADEMA
ama CCM atasema hajawahi kuhonga wala kuhongwa. Kama slaa ni msafi kama anavyotamka basi asimame mbele ya umma na athibitishe haya. Ndiyo maana hoja ya ufisadi haiendi kiutekelezaji wa vitendo. Mimi najua viongozi wa CHADEMA wanavyo tumia rasilimali za walipa kodi na misaada
ndugu waandishi,
Wapo watakaosema nimetumwa, nimehongwa, sitawapuuza, maana hao ndio walioeneza na kusambaza meseji nyingi wakitaarifu watu nimehongwa. Siasa za kutumika mimi sina, sijawahi kukaa kikao au kupewa pesa na CCM niishambulie CHADEMA. Ni vema viongozi wangu wangekuwa na hulka ya kuniuliza, vipi imekuwaje? Lakini wao hukimbilia kuwaambia wanachama – huyo mbaya sana, kapewa pesa, kala mwenyewe, mfukuzeni, hizi ni kauli au vitendo visivyo vya kizalendo kwa Taifa letu na kupandikiza chuki watu ili tuanze siasa za kuviziana. Nasema waliyosema ni uongo, uzandiki na unafiki wa Demokrasia.
Hivyo nikiwa ni kijana, bado nitafanya siasa na kikundi ninachoona kinafaa kwa wakati huo na sijutii kufanya maamuzi haya ila inaniuma kuona kazi niliyoifanya ya mageuzi inapuuzwa kwa tamaa ya wachache kukimbilia kujilipa mamilioni kama mishahara.
Nimalizie kwa kusema, nawataka wabunge wangu na hasa Joseph Mbilinyi na Msigwa – wafanye kazi ya kutekeleza ahadi zao na za chama. Tuliwaahidi wana Mbeya; bandari kavu, masuala ya Elimu, Maji, afya, ujasiliamali, amani, upendo, na kukuza vipaji vya wasanii. Lakini leo hii tunawajengea mfumo wa fujo.
Uongozi wa wilaya ya mbeya mjini ni wa mapinduzi kila kukicha kama utawala wasomalia: viongozi waliopo ni makanjanja wa kupindua wenzao kwa uroho wa ruzuku. Wamepewa kazi ya kufukuza watu uanachama na tayari wamewafukuza wengi na wanaendelea. Chama ni kufukuzana bila kufuata katiba na kuendesha mikutano ya matusi bila hoja za ujenzi wa umma mpana na bora. Wanawatuma wanachama wanishambulie eti nimehongwa.
Ujanja wa kuwateka watu na shida zao kupitia majukwaa uwe na huruma. Wakae chini waendeshe siasa za maendeleo na si kuwaza fujo na matusi. Wajifunze kutenganisha maendeleo yanayoletwa na serikali kuu kama barabara za jiji la Mbeya na Ubunge kama taasisi.
Ndugu waandishi,
Nawasihi wananchi wangu wa Jimbo la Kyela, wasinione msaliti, bali wanishauri namna ya kuimarisha harakati za kujiletea maendeleo Jimboni kwetu. Waelewe nimeshindwa siasa za sasa za CHADEMA ni siasa chafu na zenye upendeleo. Bado mimi ni mdau wa maendeleo Jimboni kwangu.
Wakati ukifika nitatangaza naingia chama gani na nitaendeleza harakati zangu za kuchochea maendeleo ya Taifa langu. Nitatimiza kazi ya uzalendo kwa nchi yangu. Wala sitaogopa kelele za wapuuzi wanaoeneza nimehongwa wakati najenga hoja. Waendelee kusambaza taarifa ambazo ingekuwa ni kazi ya CCM. Dhambi ya viongozi wa CHADEMA kuninyanyasa, kunitukana, kunidharau, na kuniundia tuhuma na kauli za kunichonganisha na umma, ipo siku itawarudi.
Naomba niwashukuru kwa kunisikiliza na salam kwa wanasiasa uchwara waliojaa siasa chafu na kazi yao ni maslahi binafsi.