Dodoma.Baadhi ya wabunge jana waliendelea kutumia fursa ya mjadala wa hotuba ya Waziri Mkuu kurushiana vijembe na maneno ya kuudhi mambo ambayo yalisababisha mivutano ya kikanuni, huku mmoja wao akionya kwamba ikiwa haki hiyo itaendelea bungeni hakutakalika.
Chimbuko la mivutano hiyo ni kauli zilizotolewa na Mbunge wa Kondoa Kusini (CCM), Juma Nkamia ambaye alimjibu Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi kwamba “haongei na mbwa bali anazungumza na mwenye mbwa.”
Kadhalika Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliwapiga vijembe viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akisema kwamba kuna wabunge ambao wana “mimba zisizotarajiwa bungeni”.
Vijembe hivyo viliendelea jioni baada ya Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje kusema Serikali iliyopo madarakani haina uwezo, haina ujuzi na imepoteza imani ya watu kutokana na kushindwa kuwatatulia wananchi matatizo yaliyopo.
Naye Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa akieleza kuwa Serikali ina tatizo kwa kuwa kuna “akili ndogo inatawala vichwa vikubwa.”
Alitumia kifungu cha kitabu kitakatifu cha Biblia cha Mithali 27:22 kinachosema kuwa “mpumbavu ukimchukua ukimchanganya na ngano kwenye kinu atabaki na upumbavu wake.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema Wenje na Msigwa walikiuka kanuni za Bunge kutokana na matamshi yao.

No comments:
Post a Comment